Monday, July 7, 2008

Nora si mwenzetu tena!

SOMA HABARI HII.

Galacha wa ukweli katika sanaa za maigizo nchini, Nuru Nassor ‘Nora’, hivi sasa si mwenzetu tena katika tafsiri ya kawaida kwa binadamu, kufuatia mabadiliko makubwa ya kitabia aliyonayo.

Nora ambaye ni mmoja kati ya mastaa wa kike wachache wa mwanzoni, kung’arisha nyota na kupambwa mno kwenye vyombo vya habari nchini, hivi sasa hatamaniki kwa vituko, hali ambayo inathibitisha ule uvumi kwamba msanii huyo ‘amedata’.
Uchunguzi uliofanywa na waandishi wetu kwa muda mrefu kidogo, ikiwemo kuongea na baadhi ya ndugu na marafiki zake, umebaini kuwa ‘mshipa wa aibu’ wa msanii huyo ulikatika muda mrefu uliopita, ndiyo maana siku hizi ‘amechetuka’, tofauti na zamani alipokuwa akionekana mpole wa sura mpaka sauti.

“Ukweli ni kwamba hatumuwezi tena, tunabaki kumuangalia tu kama alivyo. Alipelekwa hospitali na baadaye kwa waganga wa kienyeji, lakini hali yake bado inatutia simanzi,” alisema ndugu mmoja kwa sharti la kutoandikwa jina.
Ijumaa iliyopita, waandishi wetu walifanikiwa kumpiga picha msanii huyo, akiwa ‘beneti’ na polisi (inaonekana ukurasa wa kwanza) ambaye aliamua kumdhibiti staa huyo, alipokuwa akijaribu kufanya fujo kwenye kilele cha Fainali za Miss Tanzania, Kanda ya Kinondoni.

Nora, alikuwa akilazimisha kuingia kwenye viti vya VIP ambavyo gharama yake ni shilingi 30,000, wakati yeye alilipia shilingi 10,000 kwa ajili ya siti za kawaida.

Hata hivyo, ilibainika kuwa kipindi anafanya purukushani hizo, msanii huyo alikuwa amelewa kupita kiasi. Polisi alimuachia muda mchache baadaye, kwa sharti kwamba endapo angerudia usumbufu, angechukuliwa hatua kali.

Mbali na sekeseke hilo na polisi, kwa ujumla Nora alionesha utulivu ‘sifuri’ ndani ya Ukumbi wa Msasani Club, Dar es Salaam, ilipofanyika Miss Kinondoni, kwani muda mwingi alikuwa akicheza bila mpangilio na kushangilia kwa nguvu hata pale ambapo hakustahili kufanya hivyo.

Kufuatia hali hiyo, msanii mmoja anayeigiza kwenye mchezo wa Hukumu ya Tunu, unaorushwa na ITV, alijikuta akiangua kilio kwa kile kilichoonekana kuwa ni kushindwa kuamini vituko alivyokuwa akivifanya Nora.

“Yaani Nora ndiyo kawa hivi, oh my God!” Alisikika akisikitika msanii huyo (jina kapuni) ndani ya Msasani Club.

Hivi karibuni, Nora alitoa madai mazito dhidi ya wasanii wenzake, Vincent Kigosi ‘Ray’ na Blandina Chagula ‘Johari’ na kuchapishwa kwenye gazeti ndugu na hili la Ijumaa kuwa wenzi wake hao kwenye sanaa ndiyo wanaomroga na kumharibia dira ya maisha yake.

Ndugu mwingine wa karibu na Nora (jina tunalo), aliliambia gazeti hili Jumamosi iliyopita kuwa yeye na memba wengine wa familia yao, walianza kuyasoma mabadiliko ya kitabia ya msanii huyo tangu alipolimwa talaka na aliyekuwa mume wake, Marehemu Dk. William Limbe ‘Ng’wizukulu Jilala’.

“Ni hapo ndipo alipoanza kuonesha mabadiliko ya tabia mpaka kuchanganyikiwa. Hivi leo hatujui kama atapona na kurudi katika hali ya kawaida, kwani siyo mwenzetu tena, sisi tunamuachia Mungu atende miujiza yake amuokoe ndugu yetu,” alisema ndugu huyo.

Mbali na kuripotiwa ‘uchizi’, Nora aliwahi kukumbwa na skendo la kupigwa picha za utupu na kutolewa magazetini, pia hivi karibuni, alinaswa akiwa amevaa nguo bila heshima kwa kutinga suruali huku bikini yake nyeupe, ikionekana waziwazi, ndani ya Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam kwenye Tuzo za Vinara wa Filamu.
Ijumaa iliyopita, gazeti hili lilijaribu kuongea na Nora uso kwa uso, lakini msanii huyo alikimbia.

No comments: