Friday, June 27, 2008

MH! JAMANI MAPENZI ...

MAANA HALISI YA MAPENZI INAPOTOSHWA

Kwa nguvu za Mungu wangu wa mbinguni mimi ni mzima wa afya njema na ninaendelea na majukumu yangu ya kila siku vyema. Kati ya majukumu yangu makubwa ambayo napaswa kuyatimiza kila siku ni pamoja na hili la kukumbushana juu ya kuwa bora katika uhusiano na wapenzi wetu...

Kwanza kabla sijaenda mbali sana katika mada hii ambayo naamini itawagusa wengi, ni vizuri kama tutajiuliza kwa pamoja maana ya mapenzi! Mapenzi humaanisha nini hasa? Mapenzi ni hisia ambazo zipo moyoni mwa mtu kwenda kwa mwingine, hisia hizi ili ziweze kuwa mapenzi ni lazima ziwe na ukweli na penzi la dhati huku moyo ukiwa na nafasi kubwa katika hilo. Hii ndiyo maana halisi ya mapenzi. Kwamba unapoingia katika uhusiano na mpenzio hupaswi kabisa kuwa na mtu mwingine kwakuwa utakuwa unaunyima haki moyo wako.

Pamoja na ukweli huo juu ya mapenzi lakini hivi sasa maana halisi ya mapenzi imepotoshwa, imebadilishwa na kuwa nyingine. Mapenzi ya siku hizi yamejaa ulaghai mtupu, hayana ukweli, kila siku ni maumivu juu ya maumivu. Kwanini watu wanaharibu maana halisi ya mapenzi?

Kuna matatizo mengi ambayo yanaweza kutokea ikiwa utakosa uaminifu kwa mpenzi wako, wakati mwingine matatizo hayo huweza kumlenga mwenzi wako moja kwa moja bila kukusumbua wewe lakini mwisho wa siku wewe utakuja kuwa na matatizo zaidi ya hayo unayoyafanya nyuma ya pazia hivi sasa.

Unaweza kujifanya mjanja sana kwa kuunganisha wapenzi zaidi ya kumi huko gizani ukiamini huonekani na hakuna matatizo yoyote ambayo unaweza kuyapata, kumbe unajidanganya maana kuna siku utakuja kuumbuka kwa kuonekana kwako huna uaminifu!

Hivi ni kwanini maana halisi ya mapenzi hivi sasa imepotoshwa? Ni nani muanzishi wa upotoshaji wa maana halisi ya mapenzi, utagunduaje kama mpenzi wako ni msaliti wa penzi lako. Haya na mengineyo utayapata katika mada hii, unachotakiwa kufanya ni kufuatana nami katika mfululizo wa makala haya utapata kitu kipya akilini mwako.

PENZI LA KITAPELI

Wengine huwa ni tabia yao ya asili, siyo mkweli kuanzia malezi ya wazazi wake hayasisitizi juu ya ukweli, ameshazoea kufanya mambo kiujanja ujanja! Kwa mpenzi wa aina hii ni vigumu sana kudumu naye. Ni mwepesi wa kutamka maneno ya mapenzi lakini ndani ya moyo wake kuna vitu viwili, kwanza anakutamani wewe na pesa zako na wakati huo huo anatamani kuwa na bwana mwingine kwa ajili ya kuongeza kitega uchumi, hili ni tatizo!

Mwanamke wa aina hii siyo ngumu kwake kukuita majina mazuri ya kimapenzi lakini akiwa hamaanishi kutoka moyoni mwake kwamba anakupenda. Hawa wapo wengi lakini ni vigumu sana kuwagundua mapema. Hawa huharibu kabisa maana halisi ya mapenzi.


Ngoja nikuulize wewe unayemsaliti mpenzi wako, unavyomfanyia mwenzako hivyo unadhani yeye hana moyo? Hivi hujui kuwa mwenzako anakupenda kwa mapenzi yake yote na amekuchagua wewe uwe mwandani wake? Siku akijiua kwa sababu yako utakuwa katika hali gani? Hebu acha utapeli wako wa mapenzi haraka sana!

Kuwa muwazi na kama unadhani haupo tayari kuwa na mpenzi basi mwache huru atafute mwingine mwenye msimamo uendelee na mambo yako na kama ni kujiuza ujiuze vizuri lakini ukijua kuwa siku moja utakuja kuingia mahali pabaya. Achana na tamaa za muda mfupi ambazo mwisho wake ni mbaya. Huyo mwanaume anayekudanganya leo, ujue kabisa kesho hayupo na wewe na atakuwa amekuachia virusi vyako vya kutosha! Kama umeamua kujitoa sadaka ni bora ukafa peke yako kuliko kumwangamiza na mwenzako ambaye hana hatia zaidi ya penzi lake la dhati kwako.

USHAWISHI...

Hili ni tatizo lingine linalochochea kuharibu maana ya mapenzi, ushawishi ni sumu nyingine katika hili. Hapa nitazungumizia pande mbili, ya kwanza ni ya mshawishi na mshawishiwa! Naweza kusema wote wana makosa maana anayeshawishi hutumia kila njia kumpata anayemhitaji lakini wakati huo huo anayeshawishiwa kukubali wakati akijua ana mpenzi ni kosa kubwa sana. Wanaume wengi watu wazima tena wenye familia zao hivi sasa ndiyo wanaoongoza kutafuta dogodogo wakidai kuwa damu zao zinachemka! Hutumia fedha, magari na kila aina ya vishawishi ili waweze kuwanasa wasichana hao wadogo wakitafuta penzi. Sijui kama wanaume wa aina hii wanatafuta nini kwa hao mabinti? Hivi kama ukigundua mkeo anakusaliti utajisikije?

Wewe unayewarubuni wasichana ambao wapo masomoni na kuwashawishi kwa fedha zako je, kama ni mwanao ndiyo angekuwa anafanyiwa hivyo ungejikiaje? Kwanini unakuwa na moyo wa chuma kiasi hicho? Ni ulimbukeni wa ajabu sana kumuacha mkeo nyumbani halafu uanze kuhangaika na vimada, wa kazi gani kwanza? Labda unatafuta penzi shatashata, sasa si bora umfundishe mkeo akufanyie hayo unayoyapenda? Kwani umemwambia unachotaka akashindwa kukupa?

Unapaswa kubadilika ndugu yangu maana dunia ya sasa siyo ya kuchezea! Kutoka nje ya ndoa siyo suluhisho, sana sana utakuwa unayafuata matatizo mwenyewe na mwisho wa siku utauchukua Ukimwi na kumpelekea mkeo ambaye ni mtulivu!

Upande wa pili ni wa wasichana ambao hushawishiwa na watu wazima, asilimia kubwa ya wasichana wa aina hii huwa na wapenzi wao, lakini kwa tamaa ya pesa hujikuta wakijitumbikiza katika uhusiano na wanaume hao. Kwanza hivi wewe binti hujipendi? Kwanini unaiacha akili yako bila kufanya kazi kiasi hicho? Hebu jiulize, mpaka amekufuata wewe ameshatembea na mabinti wangapi kama wewe? Kitu gani kilichomvutia kwako na wewe umevutiwa na nini wakati una mpenzi wako anayekupenda kwa dhati?

Hebu chekecha kichwa chako vizuri, mpenzi wako ameshakuvisha pete ya uchumba lakini unamsaliti ukijua wazi kuwa unafanya makosa kwanini unafanya hivyo? Tamaa ya fedha ndogo ndogo itakufikisha wapi kama siyo kaburini? Acha kuudhulumu moyo wa mpenzi wako, magonjwa siku hizi ni mengi, unatakiwa kutulia na kuachana na tabia zisizofaa ili mwisho wa siku uweze kuwa bora kwa mwandani wako.

Soma zaidi katika Blog ya shaluwa: www.shaluwanew.blogspot.com


No comments: