Saturday, June 28, 2008

‘Ze Comedy’ wasalimu amri!

Na Mwandishi Wetu
Hatimaye wasanii wa Kundi la Sanaa za Uchekeshaji la Ze Comedy la jijini Dar es Salaam, wamesalimu amri kwa kubadilisha jina la kikundi chao na sasa wamelamba jina jipya la ‘Zee Komedi’

Mbali ya kulamba jina hilo, habari za kiuchunguzi zinasema kuwa wana mpango wa kubadili majina yao na kuyaongezea vionjo kibao.

Katika unogeshaji huo, habari zilizolifikia gazeti hili zinasema kuwa msanii mwenye miondoko ya kustua, Lucas Mhuville aliyekuwa akijiita Joti hivi sasa ana mpango wa kujiita Jota.

Msanii mwenye vituko vingi na bingwa wa kusoma taarifa za habari, kwa staili tofauti, Emmanuel Mgaya aliyekuwa akitumia jina la Masanja Mkandamizaji ana mpango wa kujiita Masalakulangwa.

Msanii anayeigiza kwa lafudhi ya Kihaya, Mjuni Sylivester maarufu kama Mpoki sasa kuitwa Mpokile.

Msanii mwingine anayefamika kwa jina la McRegan ambaye alitambulika kwa wapenzi wake kwa staili yake ya kutoa macho na kuuliza swali la WHY?? KWA NINI??? huenda akaitwa McManaman. Hii ni kutaka kuendeleza asili ya jina lake la mwanzo ambalo lilikuwa na ‘uzungu’ ndani yake.

Joseph Shamba ‘Vengu’ ambaye alikuwa maarufu kwa kuigiza sauti ya Kichaga na kuongea Kiingereza vizuri inapohitajika, inawezekana akatumia jina la ‘Vengi’.

Isaya Mwakilasa ‘Wakuvwanga’, aliyekuwa akimwigiza kwa ufasha Edward Lowassa na hata Rais Jakaya Kikwete inaelezwa kuwa jina lake litabadilishwa na kuwa Wakuvango.

Habari zimezidi kueleza kuwa kama ilivyo kwa jina la kikundi ambalo limebadilishwa kidogo kutoka lile la zamani, majina ya wasanii pia yamefanyiwa hivyo ili kutowapatia wapenzi wao, wakati mgumu wa kukumbuka majina.

Pamoja na kuwepo mpango huo wa kubadilisha majina, wasanii hao wanafanya kitu hicho kuwa siri hadi hapo baadaye watakapowapatia ‘surprise’ watazamaji wao.

Kitendo cha kikundi hicho kubadilisha jina kimetafsiriwa na wapenzi wa sanaa nchini kuwa ni kusalimu amri kwa agizo la COSOTA lililowataka wasiendelee kutumia majina waliyokuwa wakiyatumia kabla ya kuhamia TBC.

Mwandishi wetu alipompigia simu mmoja wa wasanii hao, Emmanuel Mgaya ‘Masanja’ ili kuthibitisha mabadiliko hayo, alikiri kubadilishwa jina la kikundi chao lakini alikanusha kubadilisha majina yao kwa sasa.

“Ni kweli tumebadilisha jina la kikundi chetu, badala ya Ze Comedy, sasa ni Zee Komedi, majina yetu hatujabadili,” alisema Masanja.

Hata hivyo, msanii huyo alisema vionjo vyao vitabaki kuwa vilivyo licha ya kutakiwa kuviacha. Hatua hiyo wamefikia baada ya kupata ushauri kutoka kwa mwanasheria wao.

Wakati zoezi hilo la kubadilisha majina likiendelea, michezo ya wasanii hao kupitia Luninga ya TBC, bado ni kitendawili kwani haieleweki lini wataanza rasmi licha ya matangazo yao kuonekana mara kwa mara katika kituo hicho.

Hatua ya mpango huo wa kubadili majina inatokana na kauli ya Afisa Mtendaji Mkuu na Mkaguzi wa Hakimiliki wa COSOTA, Yustus Mkinga kuwa Ze Comedy ilianzishwa na East Afrian Television (EAT) na kwamba kabla ya hapo hapakuwa na jina kama hilo.

Mkinga alisema kuwa wasanii wanaofanya kipindi cha Ze Comedy wana haki ya kuhama, lakini majina yao na jina la kipindi vitaendelea kubaki EAT kwani wao ndio wenye mali hiyo.

No comments: