Na Joseph Shaluwa
Mkali wa Bongo Fleva anayetesa na nyimbo za kulalamika, Lawrance Malima a.k.a Marlaw ameonesha ukomavu katika Tasnia ya Muziki wa Kizazi Kipya baada ya kutwaa tuzo mbili zilizoandaliwa za Dandu Music Awards. Marlow alikabidhiwa tuzo hizo Juni 28, mwaka huu, katika sherehe iliyofanyika katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski iliyopo jijini Dar es Salaam. Mkali huyo ambaye ndiye mshiriki pekee aliyeshinda tuzo mbili katika mashindano ya mwaka huu, alifanikiwa kutwaa tuzo ya Mwimbaji Bora wa Kiume na ile ya Wimbo Bora wa Mwaka ambapo wimbo wake wa Bembeleza ndiyo ulioshinda.
Katika kinyang’anyiro hicho, Marlaw alikuwa akitoana jasho na wakali wengine kama TID, Mzee Yusuph, Muumin Mwinjuma na Ally Kiba katika tuzo ya Mwanamuziki Bora wa Kiume. Wakati katika tuzo ya Wimbo Bora wa Mwaka, kibao chake cha Bembeleza kilikuwa kikichuana vikali na Siku Hazigandi (Jay Dee), Pembe la Ng’ombe (Dar es Salaam Modern Taarab), Mtaa wa Kwanza (Twanga Pepeta International) na Cinderella (Ally Kiba). Wakati huo huo Tuzo ya Mtayarishaji Bora wa Mwaka ilikwenda kwa Marco Chali anayewakilisha kutoka Studio za MJ Record zilizopo Masaki jijini Dar es Salaam. Tuzo ya Mwanamuziki Bora wa Kike ilikwenda kwa Judith Wambura a.k.a Jay Dee, hata hivyo, ilipokelewa na mumewe, Gadner G. Habash kutokana na mwanadada huyo kuwa nchini Uingereza katika shughuli za muziki.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment