Tuesday, August 12, 2008

KUMBUKUMBU YA COMPLEX AGOSTI 22, 2008

Wasanii kibao wa muziki wa kizazi kipya wanatarajia kumkumbuka Marehemu Simon Sayi "Complex" kupiti tamasha kubwa lenye jina la Remember litakalofanyika Agosti 22, mwaka huu ndani ya ukumbi wa Africentre, Ilala, Dar es Salaam, Christopher Lisa anashuka nayo.

Ndani ya safu hii mratibu wa tamasha hilo, George Alphonce "MC George" alisema kwamba, msanii Joan Matovolwa "Joan" ni miongoni mwa mastaa watakaokuwepo ndani ya tamasha hilo na tayari amesharekodi wimbo maalum kwa ajili ya siku hiyo.


"Joan" ambaye pia ni muigizaji wa luninga hivi sasa yupo katika mishemishe za kuitambulisha kazi hiyo ambayo ndani yake imewataja marehemu Complex na Stevie 2K, kupitia vituo mbalimbali vya redio. Wimbo huo umefanyika kupitia studio za Backyard, chini ya mtayarishaji Braton.

"Mbali na Joan, wasanii kama A.Y, Prof. Jay, Fid Q, Mwana FA, Wanaume Family, Wagosi wa Kaya, Dany Msimamo na wengine kibao wakiwemo wale waliowahi kufanya kazi na marehemu Complex watakuwepo siku hiyo, ambapo kwa heshima watapata nafasi ya kuongea mawili matatu kuhusu Complex", alisema George.


Aidha, mratibu huyo alisema kwamba, lengo la "Remember" ni kumkumbuka na kuyaenzi yale yote yaliyoachwa na marehemu kwa kuyaendeleza, kitu ambacho pia kitasaidia hata kizazi kijacho kuutambua mchango wake. Complex na aliyekuwa rafiki yake, Vivian Tilya walifariki katika ajali ya gari Agosti 21, 2005.

"Mbali na Complex, siku hiyo pia tutawakumbuka wasanii wote waliowahi kutoa mchango wao katika sanaa ya muziki nchini ambao tayari wametangulia mbele ya haki, itakuwa ni siku ya kipekee zaidi," alisema mratibu huyo.

No comments: